Posted on 3 Comments

Uhuru wa Mshairi

Mshairi amekubaliwa kutumia lugha namna anavyotaka wakati anatunga shairi.Anaweza kukiuka kanuni ambazo hutawala sarufi. Uhuru huu humsaidia kukidhi mahitaji ya kiarudhi kama vile urari wa vina na usawa wa mizani.

Uhuru wa mshairi umegawika katika vipengele vifuatavyo

  • Inkisari
  • Tabdila
  • Mazida
  • Lahaja
  • Kufinyanga sarufi
  • Kikale
  • Utohozi

Inkisari

Mshairi ana uhuru wa kufupisha maneno fulani anapotunga shairi. Anaweza kuondoa silabi fulani katika neno na kuliacha hivyo au kutumia ritifaa kuonyesha silabi imedondoshwa.

mfano:

inkisari sahihi
lopote lililopotea
nambie niambie
‘tu mtu

Umuhimu : kutosheleza idadi ya mizani/kuleta ulinganifu wa mizani.

Tabdila

Tabdila ni uhuru wa mshairi wa kubadilisha sauti za neno bila kubadilisha idadi ya mizani.

Mfano

Tabdila sahihi
mua muwa
njia njiha
toa toha

Umuhimu: kutosheleza urari wa vina

Mazida

Mazida ni uhuru wa kurefusha maneno. Neno huongezwa silabi ili kurefushwa.

Mfano

mazida sahihi
muwalimu mwalimu
jamaneni jamani
zamania zamani

Umuhimu: kuleta urari wa vina na kusawazisha idadi ya mizani.

Lahaja

Lahaja ni tofauti katika matamshi na maumbo ya maneno kwa lugha yenye asili moja. Mshairi ana uhuru wa kutumia lahaja katika utunzi wake. Lahaja ya kimvita hujitokeza sana katika mashairi ya Kiswahili.

Lahaja sahihi
mato macho
hino hiyo

Umuhimu : urari wa vina na kusawazisha idadi ya mizani katika mshororo.

Kikale

Mshairi ana uhuru wa kutumia msamiati wa kizamani. Hakuna mpaka mkubwa kati ya lahaja na kikale. Baadhi ya maneno ambayo ni msamiati wa kikale huweza kuwa lahaja pia.

kikale sahihi
hino hiyo
ola tazama

Umuhimu : urari wa vina na kusawazisha idadi ya mizani.

Utohozi

Utohozi ni uhuru wa kubadilisha maumbo ya maneno ya lugha chanzo ili yalingane na fonolojia ya Kiswahili. Mshairi hufanya kitendo cha kuswahilisha maneno ya lugha geni kama vile kiingereza.

Kiingereza utohozi
nurse nesi
one wani
school skuli

Umuhimu: kuleta urari wa vina na kusawazisha idadi ya mizani katika mshororo.

Tanbihi: kumekuwa na mjadala iwapo utohozi ni uhuru wa mshairi kwa sababu baadhi ya maneno yaliyotoholewa yamekubalika katika kamusi.

Kufinyanga sarufi

Mshairi ana uhuru wa kukiuka kanuni za muundo(muundo wa sintaksia) wa sentensi ya Kiswahili. Anaweza kubadilisha mpangilio wa maneno ,vifungu vya maneno, virai au vishazi katika sentensi.

Kuboronga sarufi sahihi
Wapitao watoto Watoto wanaopita
Kikaoni kifika kiongozi Kiongozi akifika kikaoni

Umuhimu : kukidhi mahitaji ya vina

Tanbihi

Umuhimu wa kila kipengele ujadiliwe kulingana na shairi husika.

Tazama video kuhusu makala haya

Content Protection by DMCA.com
Share this;
guest
3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
3 months ago

nice teaching

palma
palma
3 months ago

nice