Posted on Leave a comment

Maudhui ya tamaa katika Tumbo Lisiloshiba

Said A.Mohamed ni mwandishi mwenyee umaarufu mkubwa katika Fasihi ya Kiswahili. Vitabu vyake huwavutia wasomaji sana.

Hadithi fupi huwaiwaitaji wasomaji wawe makini sana ili waelewe kinachozungumziwa na maudhui. Wanufunzi hukosa mifano faafu na ya kutosha katika hadithi fupi.

Tumbo Lisiloshiba-Said A. Mohamed

Tamaa ni hamu kubwa ya kupata kitu. Mtu aliye na tamaa ni mtu ambaye hatosheki. Kutokana na maana hii tunaweza kusema kuwa mtu mwenye tumbo lisiloshiba ni mtu mwenye tamaa kwa sababu anakula na hatosheki.

Ikumbukwe kuwa   anwani Tumbo Lisiloshiba  imetumika kijazanda ikiwa na maana ya watu (wenye mali) ambao hawatosheki, wana hamu kubwa ya kupata mali zaidi.

Jitu la miraba minne lina tamaa ya chakula.Linapoingia katika mkahawa mshenzi kwa Mzee Mago linaitisha na kula chakula chote.

Kabla ya kuendeleza mjadala huu ningependa nirejelee maneno yafuatayo (tunawasaidia Wanamadongoporomoka kutegua kitendawili);

  • “Wala sitaki msaada wako dhaifu”

Kwa hivyo jitu hili linatumbua kuwa “msaada” wa Mzee Mago ni dhaifu, Mzee Mago anaishi Madongoporomoka “ wanakoishi watu wepesi wasio na mashiko”.

  • “ Nimekuja kukusaidia wewe. Nitakusaidia sana. Usiwe na wasiwasi”

Maneno haya ni kinaya. Jitu lenye tumbo lisiloshiba linamhakikishia Mzee Mago kuwa linakuja kula ardhi yake. Polisi wanatumiwa na watu wa aina hii kuwafukuza na kuwapiga wananchi wasio na hatia ili wahame katika ardhi yao.Wahame? Hapana, hawana pa kuhamia,jiji limejaa “ tukiondoshwa hapa tutakwenda wapi hapa jijini?”- maneno ya Kabwe.Watu walio nacho wanaongozwa na tamaa kwa hivyo hawawezi kuwasaidia maskini wanaoishi Madongoporomoka.

  • “Wakikubali wasikubali,itabidi leo chakula chote nikile mimi”

Wanamadongoporomoka wakubali wasikubali ardhi ya watu wasio na nguvu itanyakuliwa. Linakula chakula chote hata cha wale waliokuwa wamepanga kula hapo mkahawani.Tunatambua kuwa ardhi inayonyakuliwa, inanyakuliwa kwa lazima na watu wenye tamaa na wenyewe hawana pa kwenda “ hawajui wakimbilie wapi”

  • “Nina njaa kubwa ajabu”

Jitu hili lina tamaa, ni kweli kwa sababu lina mipango ya kunyakua ardhi ya watu wengi ambao hawana kwingine, hii si ni njaa kubwa ajabu?

  • “Nitalipa gharama zote. Nitalipa mara tatu tu …”

Tunatambua kuwa Jitu hili ni bwanyenye. Ni tamaa tu inaliongoza.Lina uwezo wa kulipa chakula chote ambacho kingewalisha watu wengi tena mara tatu. Lina mali nyingi lakini halitosheki.

  • “Kesho kama  sote tutaamka salama”

Maneno haya ni kinaya. Kila mtu aliamshwa na vishindo na vitisho vya mabuldoza na waliokuwa wamelala kutimuliwa na askari wa baraza.Jitu nalo lilifika kwa gari kubwa huku likitabasamu.

  • “ kama tutafungua milango ya nyumba zetu zinazosimama juu ya ardhi hii adhimu..”

Anawakejeli Wanamadongoporomka. Wengi hawakuweza kufungua milango yao  ya vibanda mshenzi ,vinabomolewa na askari wa baraza la mji. Je,ardhi hii ni ardhimu? Ardhi ambayo itahitaji kusafishwa, kukogeshwa na kusuuzwa?

  • “Nimekuja kula ardhi yako leo”

Ikumbukwe kuwa jitu likiondoka liliagiza kuwekewa chakula mara mbili. Kutokana na maneno haya tunatambua kuwa limefika kuhakikisha Wanamadongoporomoka wamefukuzwa ili liweze kumiliki ardhi yote.Hii ni tamaa.

Jitu hili lina tamaa ya kujiongezea mali. Jijini kumejazwa majumba na wakubwa mpaka hakuna nafasi hata ya mtu kuvuta pumzi.

Jitu hili kweli halishibi linaendelea kula tu, lina tamaa ya kuendelea kumiliki mali zaidi. Baada ya kulijaza jiji wakubwa wanataka kunyakua ardhi ya Wanamadongoporomoka.

Wakubwa wana tamaa kubwa, wanataka kuchukua ardhi ya watu maskini kwa lazima. Ardhi ya Wanamadongoporomoka inachukuliwa kwa lazima,askari wa baraza wanabomoa vibanda,kupiga na kuwafukuza watu huku wamelindwa na jeshi la polisi lilokuwa limebeba bunduki.

Lakini fujo hizi hazikuwahamisha Wanamadongoporomoka

Kutokana na uzito wa maudhui ya tamaa mifano iliyotolewa hapa au itakayotelewa inaweza kutumika kuelezea ufaafu wa anwani.

Content Protection by DMCA.com
Share this;
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments